Ujiza wa kuchora
Baba alinionesha ujiza wa uchoraji
Daddii alijiketiza mezani,
kashika penseli, na kitabu, na kifutio.
Daddii kabaki kimya,
kaanza kutembeza penseli kwa kitabu, bila kifutio.
Je, ni ujiza gani unaotendeka?
Mwana: Daddii...
Baba: Hmm...
Mwana: Unafanya nini?
Baba: Maliza Homework babaa, alafu nitakuambia.
Nikaondoa vitabu vya shule,
kunang'ana na Homework.
Lakini,
Daddii kwa umakinifu, wateleza penseli karatasini.
Laini kwa laini,
ulimwengu unajifunua.
Mwana: Daddii...
Baba: Hmm...
Mwana: Unafanya nini?
Baba: Umemaliza Homework?
Mwana: Ah, Ah.
Baba: Basi babaa maliza Homework, alafu nitakuelezea.
Nikaondoa vitabu vingine vya shule,
nikaendelea kunang'ana na Homework.
Lakini,
Daddii kwa umakinifu,
kapaka alama karatasini.
Je, ni miuijiza gani inayotendeka?
Maanake,
naona anga, na ardhi, na miti,
naona mito, bahari, na jangwa.
Kwa kweli nikitazama makini,
naona ulimwengu unajifunua.
Mwana: Daddii...
Baba: Naam...
Mwana: Unafanya nini?
Baba: Umemaliza Homework babaa?
Mwana: Ah, Ah.
Baba: hA hA! Basi si umalize Homework jameeni, alafu nitakuonyesha.
Nikaondoa vitabu vingine tofauti vya shule,
nikaendelea kunang'ana na Homework.
Lakini,
Daddii kwa umakinifu,
kabusu penseli karatasini.
Ni miujiza gani huu msee anafanya jameeni?!
Maanake,
naona wanyama, na boga, na masoko,
naona barabara, magari, reli, na lori,
naona nyumba na majengo, na dunia,
yaliyorembeshwa na binadamu.
Siamini.
Ulimwengu umeshajifunua.
Mwana: Daddii...
Baba: Naam...
Mwana: Nimemaliza Homework!
Baba: Kweli?
Mwana: Eeeehhh.
Baba: Haya, basi njo, utazame.
Tazama babaa,
jinsi penseli imebusu karatasi.
Tazama babaa,
jinsi penseli sio ya uandishi pekee.
Tazama babaa,
jinsi penseli kaweka alama karatasini.
Tazama babaa,
alama hizi zawezaumba ulimwengu.
Tazama babaa,
miujiza na uchawi yanayowezekana.
Tazama babaa,
kwani uchawi na miujiza,
yako kwako mkononi na moyoni.
Tazama na uwe makini babaa.
Kwani uumbaji wa ulimwengu,
wafunuliwa na zana, hizo hizo.
Usije kasahau, umuhimu wa somo hili.
Usije kasahau, umuhimu wa zana hizi.
Aliye na penseli, karatasi na kifutio,
aliye na guvu, na hali, ya kufunua ulimwengu.
Aliye no roho, na moyo kahisi ulimwengu,
aliye na uwezo na nia kutenda miuijiza na uchawi.
Sasawa...
Sitasahau Daddii uchawi na ujiza,
wa penseli, karatasi na kifutio.
Sijasahau Daddii uchawi na ujiza,
wa penseli, karatasi na kifutio.
K. Nzumbi Mutemi, 2026