Mama watoto, (u)siwachukue
Usiwachukue watoto mama
Ni muda kiasi umenisumbua, ati wataka kuenda mbali,
wasema kwa uchungu, ni vigumu kuishi nami.
Ati nimeleta mahatari, na majambazi,
ni vigumu kuishi nami,
“N’tachukua watoto, baba watoto, niwapeleke mbali!”
Ati n’kawakaribisha mapepo na mashetani,
wasema kwa ukali, ni vigumu kuishi nami.
N’kakuahidi, msongo wa mawazo, na wasiwasi, utuliye.
Tazama jinsi baba watoto, kakazana na kazi,
ili tuishi salama, Alsalam ealayna.
“Usiwachukue watoto, mama watoto, kawapeleka mbali!”
N’karudi nyumbani, kutopata kicheko wala sauti.
MAMA WATOTO! MAMA WATOTO!
Je mama, watoto, m’ko?
Mama watoto, usije kawachukua,
kawapeleka mbali?
Juzi ‘kaniahidi, t’tazungumza, ati ili tuelewane,
leo mimi, n’kapata nyumba bila kicheko, bila sauti.
MAMA WATOTO!
Itika mama watoto, nisije n’kalemewa na wasiwasi.
MAMA WATOTO!
Nisije n’kagundua,
watoto umewachukua, kawapeleka mbali.
Jirani-O, Jirani-O, hodi hodi jirani,
n’namtafuta mama watoto, asiyepatikana nyumbani.
Wakwe-O, Wakwe-O, shikamooni wakweni,
m’memuona mama watoto, hapatikani nyumbani.
Mama watoto, woooiiiye! Mama watoto, woooiiiye!
Kwa nini kawachukua, kawapeleka mbali.
Mawiki kadhaa yameshapita, majonzi yananilemea,
nikuulize mama watoto, ni vipi nilikukosea?
‘kaamua k'amba ni sawa, kuninyima haki ya mzazi?
MAMA WATOTO!
Nakuita mama watoto, tafadhali mama watoto,
‘sininyime haki ya mzazi, na upendo wa watoto.
N‘nakusihi mama watoto, ni nini nifanyeje,
ili niwaone, walioumbiwa na wewe.
Wafahamu mama watoto, umuhimu wa baba,
mtoto kutokuwa na babaye, milele ‘tateswa.
Mama watoto, mama watoto, jameni mama watoto,
kwa nin’ ka'chukua watoto, kawapeleka mbali.
Ni miezi kadhaa iliyopita, bila kuwaona wanangu,
n’nazidiwa na huzuni, na uchungu moyoni mwangu.
Sijasahau sauti wala vicheko, vya Thumbi na Kathembi,
nikishindiwa na kuishi, maisha naazima kwa kumbukumbu.
Mama watoto, nakuomba, mama watoto niombee,
nisamehe mama watoto, n’kawafukuza, kawapeleka mbali.
Uvumi kweli mama watoto, wakwenda Ulayani?!
Uvumulivu sina mama watoto, tafadhali 'siwapeleke mbali.
Watoto si wako pekee! Kwani ni wangu pia,
‘siwachukue mama watoto, bila upendo wa baba.
Mama watoto, Mama watoto, niliku-,
WAkosea mama watoto.
Lakini nihurumie mama watoto, niokoe mama watoto,
kwani bila watoto, mama watoto, ‘fadhali kifo, mama watoto.
Siamini ni miaka miwili, kutowaona watoto wangu,
n’na uhakika wameshakuwa, wakarefuka na kuerevuka.
N’nateseka mama watoto, kutoona watoto wangu,
zawadi za Mungu, na zawadi za uumbaji wako.
Mama watoto, kuishi kigumu,
bila upendo wao, na uumbaji wako.
Mama watoto nilikukosea, nikawakosea mama watoto,
kisha nami pia, mama watoto, n'kajikosea mama watoto.
Mama watoto, nilijaribu,
kuwa muhimu maishani mwenu.
Madhambi yangu kawakosea, madhambi yangu kanikosea,
katu’pa maisha bila mustakabali.
Mashinikizo ya maisha, kanifanya mjanja,
mashinikizo ya maisha, kanisukuma kwa shetani.
Tamaa ya pesa, na mali, kudosika na kutajirika,
kaniletea mahatari, majambazi na mashetani.
Mashetani kanichafua roho, majambazi kanivunja mwili,
mahatari kasisitisha moyo, na kudhoofisha uungano familia.
Mashetani kauua roho, majambazi kauua ubongo,
mdogo mdogo kifo cha moyo kafuata.
Mama watoto nimeelewa, nimeelewa mama watoto,
kwan’ni kawachukua watoto, kawapeleka mbali.
N’naumwa moyo mama watoto, kwamba watoto ‘tanisahau,
ndio maana, nakuomba nifanyie hii.
Mama watoto, ukiwa na nafuu,
nielezee jinsi watoto wanaendelea,
bila shaka wameshakuwa vijana.
Mama watoto, ukiwa na nafuu,
waelezee watoto wangu, jinsi walivyopendwa na babaye.
Waambie, mama watoto,
poleni watoto wangu, kuishi duniani bila baba.
Watoto wangu m’nisamehe, uzito mtaoubeba,
kuishi duniani bila baba.
Mama watoto, mama watoto,
uliwachukua, kawapeleka mbali,
basi mimi nitajichukua, nami pia nijipeleke mbali.
...
Baba watoto, watoto niliwachukua,
n’kawapeleka mbali.
Nisamehe baba watoto, kwa matendo yangu haya,
natumaini waelewa, ni muhimu usalama wa watoto.
Watoto wameshakuwa, baba ulivyowapenda wanakumbuka,
naomba utulivu wako moyo baba watoto,
watoto wako salama.
Pole baba watoto, pole sana baba watoto,
watoto kuwachukua, kawapeleka mbali.
Ilizidi baba watoto, ikabidi baba watoto,
niwachukue, kuwapeleka mbali.
...
Tunakuombea baba, ulaze mwili na upone moyo.
Tunakuombea baba, ulaze hofu na upone roho.
Ingawa uko mbali, Mwengi-ko-mbinguni,
na mbinguni si mbali, Mwengi-ko-nyumbani.
Amina, Amina, twatumaini wapumzika na amani.
Na amani pumzike nawe, daimani, Amina.
K. Nzumbi Mutemi, 2026